Na. Dezidery Kajuna
Kwa kuelewa kichwa cha mada basi ni
matumaini yangu kuwa utakuwa umeweza kujua kinachoelezwa katika mada hii. Hata
kama imekuwia vigumu kuelewa kichwa cha ujumbe huu basi utakuwa unafahamu fika
ni nini maana ya inawezekana. Bidamu wengi tuna imani katika uwezekano wa jambo
fulani kutokea. Nachomaanisha hapa ni juu ya uwezekano wa neno, kitu au jambo fulani kutokea au kufanyika kwa nguvu
za kibinadamu au kimungu. Lengo langu
hapa, si kuelezea kile kinachowezekana “kimungu”, hapana nacho nataka kueleza
hapa ni juu ya kile ambacho kwa utashi wa kibinadamu kinawezekana.
Neno “uweza” au “uwezo” bila shaka ni neno
lililotokana na neno ”weza” kwa wataalamu
wa lugha ya kiswahili wanaweza kusema, neno weza ni kitenzi kinacho maanisha kustahimili
au himili jambo fulani. Kwa uwepesi
kabisa hata maana ya neno lenyewe ni rahisi. Hivyo basi ndugu msomaji, neno
uwezo ni ile hali ya kuweza kustahimili au kuhimili jambo fulani. Ni vivyo hivyo tunaweza pata maana ya kichwa
cha mada hii yaani “ inawezekana”
Mengi yamewezekana hapa duniani kwa
sababu tu binadamu ameweza au aliweza kustahimili jambo fulani na hatimaye
akafanikiwa. Wapo wengi sana, tukianza
kuwataja basi ukurasa huu utakuwa ni
mdogo sana kunakili majina yote hapa. Kwa mifano mifupi kabisa tunaweza
kujifunza kutoka katika historia ya nchi yetu pale mwaka 1950 wakati harakati
za kudai uhuru zilipo anza napengine hata kabla ya mwaka huo, na hatimaye
iliwezekana na kwa wale walioweza kutuletea uhuru mwaka 1961. Bila shaka sote
hatuwezi kumsahau Mwalimu Nyerere pamoja na wenzake. Tukumbuke pia Jinsi Tanzani
ilivyokuwa na sauti kubwa katika umoja wa mataifa miaka hiyo ya 1970 mpaka 1985,
sauti ile na nguvu ya nchi yetu ilikuwa kubwa kwa sababu viongozi waliokuwepo
waliweza kufanya jambo fulani lililoleta sifa hapa Tanzania. Tusisahau pia
jinsi tulivyoweza kuwa maarufu kwenye soka, riadha na michezo mingine, kwa
kweli ni mafanikio yaliyobaki kwenye historia tu.
Ni rudi kwenye mada yangu, nimelazimika
kuanza na mifano ili tuelewe ni jinsi gani mambo yanavyo weza kufanyika na
yakatokea. Tanzania ni nchi ya kipekee
sana iliyobarikiwa kuwa na utajiri wa aina nyingi sana. Milima na mabonde ni
vichache tu kwa kutaja, mbuga na aridhi bora ni urembo unaotufanya kuheshimika
sana, madini, wanyama na misitu vimetufanya tuwe bora kuliko wengine bila
kusahau amani tuliyodumisha kila pande ya dunia inatamani kuwa kama sisi.
Umasikini tu ndio uliotufedhehesha na kutufanya ile heshima ipotee kwa sababu
tu tumeshindwa kufanya mambo ya maana
katika kulijenga taifa letu. Ni aibu
sana kuona kuwa tumeshindwa kuweza kufanya jambo bora kwa maslahi bora ya taifa
hili.
Natambua pia kuwa Tanzania ni nchi pia
yenye watu wengi wanaopenda kulalamika bila kuchukua hatua. Malalamiko yamekuwa
mengi kuliko uwezo wa kutatua jambo au tatizo
la msingi, nadhani naeleweka hapa. Malumbano yamekuwa wimbo na biashara
kwa wengine kiasi kwamba tumesahau wagonjwa walio katika vituo vya afya bila msaada, tumewasahau wananchi wa kinywa maji machafu
bila kupata maji salama, majambazi na vibaka nao wametumia mwanya giza nene
kuiba na kupora na kufanya mauaji kwa watu wasio na hatia kwa sababu ya kukosa
umeme, ni kwa sababu tu tumeshindwa au hatuwezi kutatua matatizo haya.
Basi naomba tutoke katika ukanda wa
kulalamika na twende kwenye ukanda unaowezekana. Nacho maanisha ni uwezo tulio
nao ambao kwa njia moja au nyingine bila shaka tunaweza kubadilika. Inzwezekana
kabisa tukawa watu wa kuheshimu uhuru wa mtu na kumuamini mtu pale anaposema
anaweza kufanya jambo fulani. Mheshimiwa rahis alipokuwa kwenye kampeni za
mwaka 2005 alisema anaweza kuleta maisha bora, tulimwamini na hatimaye tukampa
ridhaa ya kutuongoza katika nchi yetu nzuri kwa bahati mbaya ametutawala badala
ya kutuongoza kwa sababu maana ya kiongozi ni kusikiliza watu wanasemaje na
kisha kutuongoza katika kufanikisha kile tunacho hitaji.
Tazizo kubwa lililopo ni
lawama nyingi kwa Mheshimiwa rais, sidhani kama rais ana makosa, mimi na wewe
ndio wenye kosa kwa sababu tulikosa ”uwezo ” wa kutambua kilicho bora na
hatimaye tukasema ni bora tu tupate kiongozi. Kwa mara nyingine tulipata nafasi
ya kutafakari tena mwaka 2010 hatimaye tukamchagua yuleyule tunaye mlaumu kila
siku kwa sababu tu tulikosa ”uwezo” wa kuchanganua na kutambua kwa maono kule
tunakokwenda. Si kosa lake na wala
tusimlaumu Mheshimiwa rahis, mwacheni amalize muda aende tutamkumbuka kwa
mazuri na kusahu mabaya yake. Tunaweza
kuleta mabadiliko hapa Tanzania ni mim na wewe kufanya maamuzi.
Inawezekana pia, kuwa wengi wetu
hatujui kuwa maendeleo ni watu ila ukweli ni
kwamba sisi wenyewe tunaweza kuleta maendeleo mengi na chanya kama
unashindwa kuelewa nacho maanisha waulize wachina, watakuambia ni maana ya
uzalendo. Uzalendo si tu kuwa mkweli kwa yale unayofanya au kukataa rushwa,
uzalendo pia ni kujitoa kwa ajili ya mendelöo ya tafia lako. Tukumbuke uwingi
wetu ni tija pia, ila swali ni je tunatumia uwingi huu wa watu kuleta
maendeleo? Tunaweza kuleta maendeleo katika mitaa yetu, kwa kujenga mshikamano
na ushirikiano.
Tunaweza changishana pesa tukajenga darasa, tukamlipa mwalimu,
tukambadilisha mwenyekiti wa kijiji au mtaa anayefuja pesa yetu na kuleta
mwingine. Tunaweza kununua vitabu kwa idadi ya watoto wa kaya zetu. Najua
utabisha sana. Ila kumbuka kila jambo linawezekana endapo tutafanya maamuzi
yenye tija na yenye kuleta maendeleo. Unasema namaanisha nini hapa? Je
umejiuliza ni harusi ngapi mnazochangia kila wiki? Je umejiuliza ni pesa kiasi
gani unazotumia katika starehe zinazo zaa ugomvi na jamaa zako? Je haujui kuwa
maendeleo ni watu? Je haujawahi kusikia harusi imegharimiwa kiasi cha shilinigi
milioni therathini? Au unasema sio wewe uliyechangia pia katika hizo milioni
therathini? Kumbuka ”kidogokidogo ujaza kibaba”
Inawezekana kabisa tukawa na barabara
nzuri kabisa na mifereji. Utauliza je
huyu mwandishi ana akili nzuri kweli? Ndio nina akili nzuri, Kwani kokoto na
changalawe zinatoka ulaya? Nacho maanisha hapa hakina tofauti na kile
kinachotokea kule Uchina, si watu waliotumika kuleta maendeleo ambayo
yanaifanya china iwe juu kiuchumi leo hii?.
Kama hukuwahi kuongea na mchina akueleze kinachotokea kule china. Hata
Nyerere alijaribu kuleta wazo hilo, kwani tumesahau wakati alipokuwa akishiriki
ujenzi wa reli, barabara, na majengo ya hospitali na shule. Kule Ghana, rais aliyewahi kuwa madarakani
Mheshimiwa JJ Rawlings alifanikiwa
katika hili nalolizungumzia na hata leo wananchi wanatamani arudi madarakani
ila katiba hairuhusu. Inawezekana
tukajiletea maendeleo wenyewe kwam misingi ya uzalendo na kujitolea kweli kweli.
Inawezekana, tukahachana na imani za
kishirikina tukidhani kwa ushirikina tunataweza kuwa matajiri, wapi bwana!
Haiwekani ukawa na mafanikio kwa njia ya ushirikina, hizo ni imani potofu tu.
Tumefikia mahali tunaondoa roho za watu kwa sababu tunataka utajiri nani
alikuwambia kuwa inawezekana? Tunakata viungo vya albino tukiamani eti tutapata
pesa na kisha kuwa matajiri. Kama hayo yangekuwa yanawezekana basi mababu zetu
wangetufundisha na bila shaka Tanzania ingekuwa ni nchi ya kwanza kwa utajiri
duniani. Kwa maana shirika la habari la uingereza linasema katika utafiti wake
kuwa watanzania sawa na asilimia sitini na sita wanaamini katika ushirikina. Je
hii ndio sifa bora kuliko zile zilizotangulia, je sifa hi ina ile ya kuwa na
sauti katika umoja wa mataifa ipi bora? Vipi kuhusu sifa zile kuwa maarufu
kwenye soka na riadha kipi bora tukilinganisha na ushirikina huu?
Inazekana tukabadilika kimawazo na
kimatendo, tukumbuke kuwa hata viongozi tuliokuwa nao ambao siku zote
wametufanya kuwa wajinga tunaweza kuwabadilisha muda wowote. Inawezekana tukagoma
kushirikiana na kumtambua kiongozi wa aina yoyote ile kama haturidhishwi nae
kitabia, kimaamuzi, na kiuwezo katika uongozi. Ni wewe na mimi kufanya maauzi
kwa sababu inawezekana. Sitangazi mapinduzi ila naeleza uwezekano ulio katika
mikono yetu au ndani yetu.
Inawezekana tukakomesha rushwa maana
nayetoa rushwa ni mimi na wewe. Nani asiyejua kuwa rushwa ni adui wa haki?
Lakini sote tumeamua kuabudu rushwa. Mfano mzuri ni kipindi kile nikiwa
mwanafunzi pale chuo kikuu cha Dar es Salaam nilipokuwa naenda kwenye mahakama
zetu hizi, ukifika pale masijara wanataka pesa ili uweze kusainiwa karatasi kwa
mhuri wa hakimu.
Wapi kwenye katiba ilipoandikwa kuwa mahakama lazima zitoze
fedha kwa wanafunzi wanaoenda kuomba msaada huo wa kisheria mahala pale? Bila
shaka hakuna, kwa wanasheria watanisaidia kwa hili. Nacho fahamu ni kuwa kama
nikienda kwa mwanasheria wa kujitegemea anaweza omba pesa au la maana ni
haki yake, na kwa sababu analipia mhuri
ule kila mwaka ni haki yake kufanya hivyo ila si haki ya mahakama. Inawezekana
kabisa tukarikemea jambo hili na kulitokomeza kabisa pamoja na rushwa zingine
zote.
Inawezekana pia tukawa na shule zenye
majengo bora na vyoo bora. Nani asiyejua kuwa kuanzia mijini mpaka vjijini
shule hazina vyoo? Je ni kweli wanachi tumeshindwa kujenga vyoo?, hata kuchimba
shimo tu?, Inawezekana kabisa tukaleta maendeleo sisi wenyewe. Kama tunaweza
kuchimba makaburi tunashindwaje kuchimba vyoo? Au ni raha sana kuona wanafunzi
wadogo na wahalimu wakiingia vichakani kujisadia na Je mtoto wako akibakwa au
kung’atwa na nyoka huko vichakani utamlaumu nani? Tubadilike, turudi katika
enzi za kujitolea na kujitegemea kwa maana nina imani kuwa tunaweza.
Inawezekana tukabadilisha mitaala ya
elimu yetu ikawa mingine na yenye uwezo wa kuzalisha wanafunzi walio bora na
wanaoweza kujiajiri wao binafsi bila kutangatanga katika mitaa ya posta
kutafuta ajira bila mafanikio. Upungufu wa ajira umezaa rushwa, tena ruswa
zingine ni za ngono. Inauma sana ila je alaumiwe nani kwa hili? Inawezekana kabisa kutokomeza rushwa za namna
hii ila tumeshindwa kufanya maamuzi hayo tungali na uwezo huo.
Inawezekana kabisa, wanafunzi
wanaomaliza elimu ya vyuo vikuu wakakopeshwa pesa kutoka katika benki
mbalimbali hapa nchini na hatimaye wakajiajiri. Lakini je wamepewa elimu ya kujiali?
Je serikali inawasaidia kisheria kupata mikopo bila rushwa au riba kubwa? Nani wakuwatetea kama sio mim ina
wewe? Inawezekana mim ina wewe tukaleta maendeleo, tukubaliane katika hili. Kama
tatizo ni uongozi basi tujiulize kabla ya maamuzi, ni nani anaweza kutuletea
mabadiliko ya kweli?
Inawezekana kabisa tukaishi katika
jamii yenye amani bila kubaguana kwa misingi ya dini au kabila. Tumeacha watu
wachache wanachezee amani na mshikamano wetu kwa kutubagua kwa misingi ya dini na
ukabila. Hili la dini ndilo swala muhimu na nasisitiza kuwa inawezekana kabisa
tukaishi katika jamii ambao hatutatambuana kwa misingi ya dini au kabila bali
kwa misingi ya michango katika kuleta maendeleo. Tutamjua mvivu asiyefanya
kazi, asiyepeda ushirikiano, mla au mtoa rushwa, mwizi au jambazi na makundi
mengine yasiyo faa katika jamii yetu na si nani ni muislamu au mwikristo.
Japo yapo mengi yanayowezekana tatizo
ni maamuzi, hatujafanya maamuzi na sijui tunangoja nini. Tubadilike, kama wewe
ni kijana badilika na tambua kuwa inawezekana ukawa na maisha bora bila kutemea
mtu mwingine, wazazi pia wanaweza kuleta maendeleo kwa kusisitiza kujituma,
kufanya kazi kwa bidii, kupunguza lawama, kujitoa katika shughuli za maendelo
na hata kuubadilisha uongozi usiofaa. Tubadilike, tufikirie, tufanye maamuzi
yaliyo na tija kwa maendeleo ya taifa letu.
No comments:
Post a Comment