Friday 25 March 2016

HESHIMA HAINA UMRI!

Na. Dezidery Kajuna.

Ni asubuhi ya saa tano, natoka ndani ya nyumba ninayoishi katika mtaa huu wa Prästgatan hapa nchin Swedeni tayari kwa ajili ya kwenda shule maarufu kwa jina la SFI  (Svenskundervisning för invandrare) kwa lugha ya kiswahili ikiwa na maana ya elimu ya lugha ya kiswidi kwa wahamihaji au wageni. Ni shule mahususi kabisa kwa ajili ya wale wanao penda kujifunza lugha hii ya kiswidi ili iwe rahisi kwao kuwasiliana na wenyeji.

Sababu kubwa ya wageni kujifunza lugha hii ni muhimu kwani lugha itumikayo katika nchi hii ni kiswidi kila utakapokwenda hapa nchini Sweden. Ni tofauti na nchi nyingine kama Uingereza, Marekani na Australia ambako lugha muhimu ni kiingereza.  Tofauti kabisa na Sweden, Norway, Finland, Ujerumani, Denmark na nchi nyingine ambako lazima usome lugha yao kwa mawasiliano ya kawaida katika jamii zao. Jambo zuri ni kuwa katika nchi hizi ofisi zote za serikali pamoja na vyuo vyote vinatumia lugha ya kiingereza kwa ajili ya wageni na lugha yao kwa ajili ya wenyeji.

Hali ni tofauti kabisa hapa nchini Sweden kwani lugha kama ilivyo mahala pengine ni muhimu kwa mawasiliano. Serikali ya Sweden kupita halmashauri zake zinatoa fursa ya bure kwa watu wote, haijalishi wewe ni mkimbizi, mhamiaji haramu au ni mgeni wa kawaida kama vile mwanafunzi au mtalii kujifunza lugha ya kiswidi

Makundi hayo yote yana haki ya kupata fursa ya kusoma kiswidi bure bila kutoa senti mfukoni mwako. Cha muhimu ni kuwa na namba ya uraia, hili ni jambo geni sana Tanzania, na sidhani hata kwa  miaka ishirini ijayo kama tunaweza kufikia hatua hii ambayo wenzetu wa Kenya labda wanaweza kuwa wamefikia.

Ukungu ni mwingi barafu likiwa limepukutika sana na nimevaa viatu si kama hivyo navyotumia nikiwa natoka kwa mama Mtey (mwenye nyumba) hapo ubungo kwenda mjini hasa posta ya zamani kutafuta kazi katika maofisi.

Kipindi cha baridi na haswa kipindi cha barafu inakulazimu kuvaa viatu maalumu kwa ajili ya kuweza kutembea salama katika barafu ili usianguke na wala miguu isiweze kuganda kutokana barafu.

Wakati huo huo umevaa makoti mazito kwani baridi hili si mchezo kama haukupata mlo wa kutosha lazima tumbo lilalamike. Katika mtaa huu kila unayekutana nae anahema huku akitoa moshi mdomomi si kwamba wanavuta sigara la hasha! Ndilo baridi lilivyo mwili unakuwa umepigwa baridi kiasi cha kufanya mvuke utoke ndani ya kinywa.

Najikongoja taratibu, navuka barabara huku ni kibonyeza kitufe chekundu ili taa za barabarani ziweze kisimamisha magari nami nipite niende zangu shuleni. Nakatiza uwanja bila shaka nimefika shuleni, wanafunzi wachache wapo nje wanavuta sigara maana huku ni kawaida sana kutokana na hali ya hewa.

Nalazimika kusafisha viatu vyangu kwanza ili niingie ndani maana barafu limeganda kwenye viatu vyangu mithili ya matope ya soko la Tandale. Naingia ndani ya jengo la shule kabla sijaingia darasani napita sehemu yenye komputa nyingi mahsusi kwa jaili ya wanafunzi ghafla nasikia mtu anaita Eric! Eric! Eric!

Kisha nageuka, kuangalia nyuma naona mtu wa makamo sana akiwa amesimama karibu na komputa akiwa na begi kubwa mithili ya msafiri nami namsogelea nisikilize anasemaje.

Kumbe wakati anaita Eric! Alikuwa ananiita, nilimwitikia kwasababu Eric ni rafiki yangu wa karibu na ni mwanafunzi mwenzangu kutoka Ghana bila shaka nilijua mzee huyu amenifananisha na rafiki yangu. Kama utamaduni wangu nikamsogelea, tukasalimia na mara hii anaonyesha heshima sana kwangu japo haukuwa utamaduni wake kumbe anashida, jana yake alikuwa amelala nje kwa maana shirila la nyumba lilimfukuza na baridi hii nilimwonea huruma sana.

Cha msingi nilitaka kusikiliza anasemaje. Ananiuliza kama naweza kumsitiri au kama namjua mtu yeyote mwenye chumba cha ziada maana mtu aliyekuwa anaishi nae na ambaye ndie aliyekuwa mpangaji halali amefariki na hivyo kisheria hapa nchini Sweden lazima uondoke maana kimkataba hautambuliwi. Jawabu nililo mpa ni kwamba sina sehemu ya kumsitiri kwa muda ule maana na mimi naishi mtu na kwa wakati huo sikuwa na taarifa juu ya mtu mwenye chumba cha ziada.

Kwa msaada tu nampa majina ya kampuni mbali mbali zinazohusiana na vyumba vya kupanga. Kisha namtakia kila lakheri, naondoka zangu nikimuacha na masikitiko maana labda alidhani ndo tatizo limeisha, ukweli maisha hapa ni magumu hasa ukiwa huna mahala pa kuishi, kwa kweli ni kazi.

Kipindi hiki cha baridi kali kimekuwa hatari huku ulaya.  Ulaya Mashariki, watu wengi zaidi ya mia nne wamepoteza maisha wengi wao wakiwa wazee na wale wasio kuwa na makazi maalumu. Baridi hili kama hauna kipoozeo (heater) basi ujue unakufa maana barafu hili likiambatana na baridi mara nyingi upelekea damu kuganda na hivyo upelekea maumivu katika sehemu mbali mbali nyingi za mwili hasa kwenye vidole na kwenye paji la uso.

Mzee huyu kwa jinsi nilivyomuona basi atakuwa amepata taabu kweli katika usiku uliopita. Mzee huyu si mzungu jamani! Ni mtu mweusi kama mimi, yeye anatoka Kameruni, nchi yenye mchezaji soka maarufu wa kimataifa Samuel Eto’o! Aliwahi kufika Tanzania na wasakata kambumbu wenzake.

Huku, Sweden, kila katika mji utakaoenda hautakosa mkameruni, maana ni wengi sana mithili ya wachagga ambao wametapakaa kila mkoa  Tanzania wakifanya biashara. Ila wakameruni hawa hawafanyi biashara, wao wapo huku kwasababu za kimaisha. Kameruni maisha ni magumu sana na hivyo wengi wanazamia huku na sehemu zingine za Ulaya. Uzuri  wakameruni ni uwezo wao katika lugha, wanaweza kuzungumza lugha ya kiingereza na kifaransa kwa ufasaha sana. Na ni wa watu wanaojituma sana katika kufanya kazi.

Si kwa mazuri hayo tu bali nao wanaubaya wao, kwa mtazamo wangu ni watu ambao wanaubaguzi sana, wabinafsi, lakini cha kushangaza sana ni kwamba wanadharau sana watu kutoka Afrika ya Mashariki. Maana wanaona uchache wetu hapa nchini Sweden ina sehemu zingine za Ulaya basi wanadhani sisi si watu wakujituma, ni waoga, na hatujui lugha.

Tuendelee na mzee wetu, basi mzee huyu ni mmoja kati wa ya watu wanaodharau sana vijana, hasa wa kiume.  Mara nyingi huongea vizuri na vijana wa kike hasa wanaotoka bara la Afrika. Hata wakameruni wenzake huwadharau pia ndio maana hakuweza kupata msaada kutoka kwa wakameruni hao kwa maana wanamfahamu sana.

Bila shaka walimtenga kwa sababu ya dharau zake!

Kwa sababu ni wa makamo basi alidhani yeye ni bora kuliko wadogo la hasha! Hiyo si sababu kwa maana inawezekana kijana mdogo akawa na hekima kuliko mtu mzima nikakumbuka msemo wa Kiswahili;  ”mtu mzima hovyo”!

 Si watu wote wazima wanahekima wengine ni hovyo kweli kweli! Cha msingi nachodhani ni muhimu ni heshima, mdogo aheshimu mkubwa na kubwa afanye vivyo hivyo kwa wadogo hapo maisha yakutakuwa na amani vinginevyo vijana watacharuka. Hawana simile vijana wa siku hizi ati.

Heshima ni alama ya upendo pia, maana kama hauna heshima kwa mtu mwingine maana upendo kwa mtu yule imepotea .

Ni muhimu kujenga heshima kama kweli tunapenda upendo uwe kati yetu. Jamii ya Tanzania kwa sasa inatazamwa kama jamii yenye maadili yaliyoporomoka sana kupita kiasi. Vijana wadogo wanatukana wazazi wao, wanabaka walimu, wengine wamepotelea katika matumizi  ya madawa ya kulevya, vitendo wizi na ujambazi na wengine kwenye biashara ya ngono.

Heshima ni jambo la muhimu sana, kwani haijalishi wewe ni nani na umri gani. Kwa sisi waafrika utamaduni wetu unatufunza kuwa watu wenye heshima mara zote kwa watu wazima na wadogo. Tunahitaji kuwasaidia walimu kuanzia shule za awali, msingi, sekondari mpaka vyuo kuimarisha na kusisitiza heshima, upendo na kujitoa kwa ajili ya manufaa ya jamii. Hivi vyote vikipotea basi hata uzalendo hautakuwepo kamwe!

Tusibaki kuwa watu wa kulalamikia rushwa, uongozi uliodorora na maendeleo duni. Hivyo vyote uanzia nyumbani kwa wazazi na watoto. Lazima kaya zetu zijengwe na upendo, uzalendo na heshima ili taifa liwe na watu wa aina hiyo. Bila shaka wale walio viongozi bora leo hii hapa Tanzania na sehemu nyingine duniani wana historia nzuri toka huko walikotoka wangali watoto na hatimaye baba au mama wa familia. Tubadilike na heshima tusisitize kwa rika zote!



No comments:

Post a Comment